Wanafunzi watatu waliotiwa mbaroni wiki iliyopita kwa tuhuma za kumkejeli raisi wa Burundi Pierre Nkurunziza kupitia kwa michoro katika madaftari yao wameachiliwa huru.
Kwa mujibu wa waziri wa haki wa nchi hiyo Bwana Aimee Laurentine Kanyana aliyekuwa akizungumza na wanahabari, wasichana hao wenye umri wa miaka 15, 16 na 17 wameachiliwa huru kwa sasa.
Waziri huyo aliwaomba wazazi kuwaelekeza wanao vyema.
“Tunawaomba wazazi kuwapa wanao mafunzo mema kwa kila wanachojishirikisha nacho. Kadhalika, ningependa kuwaonya wanafunzi wetu kuwa yeyote ambaye amefikisha umri wa miaka kumi na tano au zaidi anaweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria iwapo atapatikana akifanya uhalifu wowote ule.” alisema Bwana Kanyana.
Kukamatwa kwa wanafunzi hao kulikashifiwa katika mitandao ya kijamii haswa Twitter kwa kutumia hashitegi #FreeOurGirls.
Wengi wanaamini kuwa mchango wao ndio uliopelekea wasichana hao wenye umri mdogo kuachiliwa.
Kulikua na hofu kuwa wasichana hao wangefungwa gerezani kwa miaka mitano.
Soma:Wanafunzi Watatu Nchini Burundi Wakabiliwa Na Kifungo Gerezani Kwa Kumchora Rais Nkurunziza Kikejeli
Vyombo vya habari nchini Burundi viliripoti kuwa wanafunzi hao walikamatwa na wengine wanne, ambao waliachiliwa baadaye katika hali tatanishi.
Sio mara ya kwanza nchi hiyo imejipata kwenye kurunzi la kimataifa kwa kuwakamata wanafunzi wanaokejeli kiongozi wa nchi.
Mnamo mwaka wa 2016, vyombo vya dola nchini humo viliwakamata wanafunzi wanane wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumkashfu Rais baada ya kuchora michoro isiyofaa dhidi yake.
Watetezi wa haki za kibinadamu nchini humo wamekashifu utawala wa Rais Nkurunziza kwa wanachokitaja kuwa unyanyasaji wa haki za wanafunzi wasiokubaliana na uongozi wake.
Email your news TIPS to Editor@kahawatungu.com or WhatsApp +254707482874. You can also find us on Telegram through www.t.me/kahawatungu
Email your news TIPS to Editor@kahawatungu.com or WhatsApp +254707482874